Polisi wazingira nyumba ya Askofu Gwajima usiku
Jeshi la Polisi kwa mara nyingine Jumatano hii ilizingira nyumba ya Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima, kwa kile lilichodai kuwa lilifika kufanya uangalizi
Akizungumza kwa simu na gazeti la Mtanzania jana, Askofu Gwajima alikiri polisi hao kumfuata nyumbani kwake na hivyo kulazimika kumtafuta wakili wake mara moja.
“Ni kweli walikuja wakiwa na gari la polisi, lakini walipofika nami nilimpigia mwanasheria wangu ambaye aliniambia tuwaulize wametumwa na nani na kama wana ‘search warrant’ (kibali cha kufanya upekuzi) au ‘arrest warrant’ (kibali cha kukamata),” alisema.
Aidha Askofu Gwajima alisema walipowauliza, walimtaja Afande Kingai kama ndiye mtu aliyewatuma, lakini hawakuwa na kibali chochote. Kwa mujibu wa Askofu Gwajima, mwanasheria wake alifanya mawasiliano ya simu na Afande Kingai ambaye amepewa jukumu la kuwafuatilia wale wote waliotuhumiwa katika sakata la dawa za kulevya na kumuuliza sababu za kumfuata nyumbani.
“Afande Kingai amemweleza mwanasheria wangu kuwa walikuwa wamekuja kwa ajili ya ‘observation’ (uangalizi) tu, kwahiyo mwanasheria wangu akasema kama ni ‘observation’ tu tusiwaruhusu kuingia ndani kwa sababu sheria ya hivyo hakuna, na sisi tumewazuia hawakuingia ndani,” alisema Askofu Gwajima.
Askofu huyo kupitia ukurasa wake wa Instagram ameiweka habari hiyo.
Comments
Post a Comment